Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, August 14, 2011

TSJ yaandaa mashindano ya urembo;


SERIKALI ya wanafunzi ya Time School of Journalism (TISJOSO) kwa kushirikiana na kampuni ya kizalendo ya Zealot Entertainment Agency imeandaa mashindano ya urembo ya kumtafuta mshindi na mwakilishi ya kinyang’anyiro cha Miss na Mr TSJ 2011.

Shindano hilo litafanyika katika hafla ya Welcome First Year Special Bash ambayo imelenga kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa ngazi zote kuanzia Basic Certificate, Advanced Certificate na Diploma kwa mwaka huu.

Hafla hiyo ya kuwakaribisha mwaka wa kwanza ambayo itapendezeshwa na mashindano haya inatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 3 Septemba mwaka huu katika maeneo ya Jangwani Sea Breeze Mbezi beach.

Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na serikali kwa ajili ya washiriki na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo, Waziri wa Michezo wa TISJOSO na mratibu wa mashindano hayo Bw. Frank Aman alisema mashindano ya mwaka huu ni mashindano rasmi na yako tofauti na mashindano yaliyowahi kufanyika hapo awali.

Bw. Aman alisema kuwa mashindano yaliyokuwa yakifanyika mwanzoni yalikuwa hayana tija kwa washiriki kwani hayakuwawezesha kupiga hatua yoyote ya kuendeleza kipaji hicho licha ya kuwa kuna baadhi ya waliofanikiwa kuendelea katika tasnia hiyo kama Lillian Andrew ambaye aliweza kushirirki katika kinyang’anyiro cha Miss Tabata 2010 na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu.

“Tunatarajia kuyaboresha mashindano haya na mwaka huu kutakuwa na zawadi nzuri sana kwa kuwa tumeweza kuwa na mawasiliano mazuri na baadhi ya kampuni ambazo zinaelekea kudhamini mashindano haya,”alisema Bw. Aman.

Aliongeza kuwa kamati yake pamoja na serikali ya wanafunzi inajaribu kutafuta mahusiano mazuri na waratibu wa mashindano makubwa ili kutoa nafasi kwa TSJ kuwa na warembo wanaowakilisha chuo hasa kwa Miss Tanzania ambayo ni mashindano makubwa yanayoendelea.

“Tutaboresha mashindano haya na mwakani tunaamini tutapata nafasi ya kuingia katika mashindano ya Miss Tanzania ingawa kwa mwaka huu tumechelewa kwa sababu tayari wako kambini wakijiandaa na fainali za mashindano hayo,” aliongeza Bw Aman.

Mpaka hivi sasa washiriki waliojitokeza ni 11 na tunazidi kuwahimiza wajitokeze kuchukua fomu ili washiriki katika mashindano hayo na wao watambue kuwa mashindano haya pia mshindi hupatiwa cheti cha heshima cha utambulisho ambacho mbali na zawadi pia kitampa nafasi ya kuongeza na kuonyesha ushiriki wake katika mashindano hayo.

Tunatarajia kuwa washiriki hawa wataingia katika mazoezi ya maandalizi ya shindano hili wiki mbili kabla ya tukio na siku tatu kabla ya tukio tutatangaza zawadi za washindi watakao ingia katika fainali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo fupi Waziri wa Habari wa serikali ya wanafunzi TISJOSO Bi Jestina Joseph, alisema mbali na mashindano hayo pia katika sherehe hiyo kutakuwa na mashindano mbali mbali ambayo yatatoa nafasi kubwa kwa wanafunzi kufurahia hasa kuwaweka karibu na wanafunzi ambao wameingia chuoni.

“Lengo la sherehe hii ya Welcome First Year Special Bash kwa mwaka huu ni kuwaweka wanafunzi karibu na pia kujijenga kisaikolojia kwani michezo hujenga na kujumuika pamoja katika hafla hii itatuwezesha kuwa na ushirikiano wa kutosha,” alisema Bi Jestina.

Aliongeza kuwa pia sherehe hii itakuwa sehemu mojawapo ya kusherehekea ushindi uliopatikana katika mashindano ya taaluma ya utangazaji yaliyofanyika hivi karibuni katika chuo cha Royal College of Tanzania (RCT) na TSJ iliibuka mshindi wa mashindano hayo.

“Tunaamini mashindano haya yatakuwa endelevu ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kushindanishwa kujenga uwezo na ubunifu katika taaluma hii ya uandishi wa habari na utangazaji,” alisema Jestina.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...