MKE WA HAYATI Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere amewataka wake wa viongozi kutambua dhamana walizonazo na wajibu walionao kwa jamii ambayo wenzi wao wanaiongoza.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumamosi, Februari 25, 2012) wakati alipokuwa akiwashukuru wake wa viongozi 25 ambao walifika nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam ili kumjulia hali na kumpa tuzo ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.
Mama Maria amesema kuwa wake wa viongozi kunawafanya wakutane na changamoto nyingi lakini pia akawataka watambue kuwa Taifa limewapa fursa ya kuelewa mengi ambayo kama wangekuwa wanawake wa kawaida tu wasingeweza kujua mambo hayo.
“Unapokuwa mke wa kiongozi unapata changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutoa dira kwa wengine... unapaswa kufikiri kwa niaba ya wengine iwe ni kwenye ujasiriamali, elimu, afya au masuala ya kijamii hasa namna ya kukabili changamoto za akinamama na watoto,” alisema.
“Unapokuwa mke wa kiongozi unapaswa kumshukuru kwa kuwa umepewa fursa ya kuwaongoza wengine, umepewa fursa ya kukomaa na mawazo yanakua kwa haraka kule wengine wasio na fursa kama yako,” alisisitiza.
Alisema inawezekana watu wa nje wakawaonea wivu kuwa wamepata bahati ya kuolewa na viongozi lakini wajibu wao mkubwa siku zote uwe ni kuwaombea wenzi wao na wale wanaowaongoza. “Msichoke kumuomba Mungu kwa sababu ninyi ndiyo mna kazi kubwa, mnasimama kwa niaba ya Taifa... lolote likitokea linawakumba na ninyi pia,” aliongeza.
Mapema, akitoa salamu za ujio wao, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alisema wameamua kumpa tuzo ya heshima Mama Maria Nyerere kwa sababu wanatambua mchango wake wakati aliposhiriki bega kwa bega na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye harakati za uhuru wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya wake wa viongozi mbalimbali wa kitaifa 25 ambao aliongozana nao, Mama Pinda alisema tuzo waliyompa imeandikwa “Hongera Mama wa Taifa” ikiwa ni kuthamini mchango wake. Tuzo hiyo ina umbo la ramani ya Tanzania, ina nembo ya miaka 50 ya Uhuru pamoja na picha ya Mama Maria Nyerere.
Baadhi ya wake wa viongozi walioambatana Mama Pinda ni wake wa Marais wastaafu Mama Sitti Mwinyi na Mama Anna Mkapa, Mke mkubwa wa Makamu wa Rais, Bi. Zakia Bilal, Mama Salma Omar (mke wa marehemu Dk. Omar Ali Juma), Mama Hasina Kawawa, na wake wa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu wakuu
No comments:
Post a Comment