Mbio za 10 za Kilimanjaro Marathon ambazo zimepangwa kufanyika Februali 26 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro zimepata msisimko mpya baada ya wanaridaha nyota wa Tanzania na wale wa nje ya nchi kuthibitisha kushiriki.
Katibu Mku wa Chama cha Riadha chini, Julius Musomi aliwataja baadhi ya wanariadha nyota kutoka Tanzania kuwa ni Andrea Silvini, Daudi Joseph, Getuli Bayo na Kegera Humay ambao wataungana na wanariadha wengine wa ndani na nje ya nchi kuchuana katika mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa wanaume za kilometa 42.195.
Kwa upande mwingine, Sarah Kavina, Banuelia Bryton na Rebecca Kavina ni miongoni mwa nyota wa Tanzania watakaochuana na wenzao kutoka ndani na nje ya nchi katika kuwania tuzo mbalimbali kwenye Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa wanawake za Kilometa 42.195.
Aidha, wanariadha Fabian Joseph, Damian Chopa, Faustine Musa na Mary Naali ni miongoni mwa majina maarufu katika riadha yaliyothibitisha kushiriki kupitia kundi litakalochuana katika Mbio za Nusu Marathon (Half Marathon) ambazo zitaanzia kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi(MUCCoBS).
“Wanariadha wetu wote ni wenye viwango vya kimataifa….Wakimbiaji wote katika kundi la wanaume ni wale wenye uwezo wakufika mstali wa mwisho ndani ya muda usiozidi saa 2 na dakika 10 (2:10) huku wakimbiaji katika kundi la wanawake ni wale wenye uwezo wakufikia mstali wa mwisho katika muda wa chini ya 2:30…..Tunatumbua kuwa wanariadha kutoka Kenya watatoa changamoto kwa wanariadha wa hapa nchini lakini kila mtu yuko tayari kuikabili changamoto hiyo vilivyo,” alisema Musomi.
Andrea Silvini ni bingwa wa mbio za Kilimanjaro Marathon za mwaka 2007 na pia ni mshindi wa mbio za Pune Marathon zilizofanyika mwaka 2008. Banuelia Brighton naye alishinda katika Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon mwaka 2007 kwa upande wa wanawake na aliibuka kinara katika mbio za Amani za Kigali zilizofanyika nchini Rwanda mwaka 2009.
Banuelia pia alishika nafasi ya pili kwenye Mbio za Kampala Marathon zilizofanyika nchini Uganda mwaka uliopita.
Katika mbio za Nusu Marathon, Fabian Joseph ndiye anayeshikilia rekodi akiwa ameshinda mbio za nane za Kilimanjaro Marathon zilizofanyika mwaka 2010 akiwa ametumia saa moja, dakika tatu na sekunde hamsini na tisa (1:03:59),hivyo alifanikiwa kuvunja rekodi iliyowekwa na Mtanzania mwingine Damian Chopa ambaye alishinda mbio hizo mwaka 2008 kwa rekodi ya 1:04.43.
Joseph pia ana arekodi ya kushinda mbio za Nusu Marathon za Dunia zilizofanyika katika jiji la Edmonton, Canada mwaka 2005 akiwa ametumia 1:01:08, huku chipukizi, Mary Naali, akiwa ni mshindi wa mbio hizo zilizofanyika Viena, Australia mwaka 2010 . |
John Addison, mkurugenzi mku wa kampuni ya Wild Frontiers, inayoandaa Mbio za Kilimanjaro Marathon alisema hivi karibuni kuwa takribani wakimbiaji 5000 kutoka mataifa 40 ya mabara sita wanatarajia kushiriki katika maadhimisho ya kumi ya Mbio za Kilimanjaro Marathon.
Wale mbao hawatashiriki katika mbio za kilometa 42.195 za Kilimanjaro Premium Lager na zile za nusu Marathon watajaribu bahati yao ya kushinda katika mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run. Watu wenye aina ulemavu wa aina tofauti, nao watapata nafasi ya kushindana kupitia Mbio za Nusu Marathon za Gapco (Gapco Disabled Half Marathon 2012). Kwa mujibu wa John Addison, idadi ya wanariadha wanaojisajili kwa kupitia tovuti ya Kilimanjaro Marathon ambayo ni: www.kilimanjaromarathon.com inazidi kuongezeka siku hadi siku. Hata hivyo, huduma ya kujisajili kupitia tovuti hiyo itakoma kesho kutwa, Ijumaa, Februari 17, 2012.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alisema hivi karibuni kuwa zawadi ya fedha kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu katika mbio za mwaka huu zimeongezeka kwa asilimia 100.
Jambo kama hilo pia limefanyika kwa washindi wa mbio za nusu marathon, huku Kampuni ya Vodacom pia ikitangaza kutoa zawadi nyingine kwa makundi yote ya wanawake na wanaume ikiwa ni pamoja na mshiriki mdogo na mwenye umri mkubwa zaidi katika mbio za Vodacom 5km fun run.
Kwa upande wa Kampuni ya Gapco, pia itatoa zawadi kwa makundi ya aina nne tofauti yaliyoko ndani ya Mbio za Nusu Marathon za watu wenye ulemavu za Gapco za 2012.
Mbali na Kilimanjaro Premium Lager, GAPCO Tanzania na Vodacom Tanzania, wadhamini wengine kwenye mbio hizo ni CFAO Motors, Tanga Cement, TanzaniteOne, Keys Hotel, Precision Air, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, Southern Sun, KK Security, Standard Chartered Bank na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Waandaaji wa mbio hizi ni Kampuni ya Wild Frontiers ya Afrika Kusini ambapo kwa hapa nchini zinaratibiwa na kampuni ya Executive Solutions huku Chama cha Riadha Tanzania (RT), Chama cha Riadha cha Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Hoteli ya Keys zimekuwa zikisaidia katika masuala ya ufundi na mipango ya usafirishaji watu
No comments:
Post a Comment