UTANGULIZI
Mnamo mwaka 2008 Serikali ilitunga na kupitisha Sheria Na. 8 ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii. Sheria hiyo ilianza kutumika rasmi tarehe 1 November 2009. Pamoja na mambo mengine sheria hii imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA). Jukumu kuu la Mamlaka hiyo ni kusimamia shughuli zote za Hifadhi ya Jamii nchini ikiwa ni pamoja na mifuko yote ya Hifadhi ya jamii (PPF, NSSF, PSPF, GEPF, NHIF na LAPF).
MAMLAKA YA USIMAMIZI NA UTHIBITI WA HIFADHI YA JAMII
Tunapenda kuarifu Umma kwamba serikali imekamilisha kazi ya kuunda Mamlaka iliyotajwa hapo juu ikiwa ni pamoja na kuteua Mkurugenzi mkuu, Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
UANDIKISHWAJI WA WANACHAMA
Hivi karibuni limejitokeza tatizo la wafanyakazi wapya kuandikishwa katika zaidi ya Mfuko mmoja wa Pensheni au wanachama wa Mfuko mmoja kuhamia Mfuko mwingine. Hii ni kinyume cha sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Sheria Na. 8 ya mwaka 2008.
Kufutia hali hiyo Mamlaka inatoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Kwa mujibu wa kifungu cha 29 (1), (2) na (3(a)) ni kosa na ni kinyume cha Sheria kwa Mfuko wowote wa Pensheni kuandikisha wanachama waliokwisha andikishwa na Mfuko mwingine.
Kwa mujibu wa kufungu cha 30 cha Sheria ya Usimammizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, mfanyakazi ambaye hajawahi kujiunga na mfuko wowote wa Pensheni au anayeajiriwa kwa mara ya kwanza anao uhuru wa kuchagua mfuko wowote kati ya mifuko tajwa hapo juu. Hii ina maana mfanyakazi anapaswa kuwa mwanachama wa Mfuko mmoja tu wa Pensheni.
Utaratibu wa kumwezesha mwanachama kuhama toka Mfuko mmoja kwenda Mfuko mwingine unaandaliwa. Wanachama wote wanaohitaji kuhama kwenda Mifuko mingine wanashauriwa kusubiri hadi utaratibu wa kuwezesha kuhamisha mafao ya wanachama utakapokamilika.
Kwa taarifa hii Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii inaagiza yafuatayo;
Waajiri wote katika utumishi wa umma na sekta binafsi wanapaswa kuzingatia matakwa ya sheria hii kwa kuwapa fursa watumishi wapya kuchagua mifuko wanayoitaka.
Vyombo mbalimbali kama Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD), Idara ya Utumishi wa Umma (CSD), Idara ya Utumishi wa Serikali za Mitaa (LGSD) Idara ya Utumishi wa zimamoto (FRSD), Idara ya Utumishi Afya (HSD) na vyama mbalimbali vya wafanyakazi vizingatie pia masharti ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwenye maeneo yao.
Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii kuzingatia matakwa ya sheria hii wakati wa kuandikisha wanachama wapya.
Aidha, Mifuko yote iliyoandikisha wanachama wake kinyume na matakwa ya sheria hii mara baada ya Sheria kuanza kufanya kazi (tarehe1 Novemba 2009) kurekebisha makosa hayo mara moja.
Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutohama kutoka Mfuko mmoja kwenda Mfuko mwingine hadi taratibu husika zitakapotolewa
Imetolewa na;
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846
Dar-Es-Salaam
Tanzania
No comments:
Post a Comment