Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, June 30, 2010

KESHO NI KUANZWA RASMI UTEKELEZAJI WA SOKO LA PAMOJA LA AFRIKA MASHARIKI KWA NCHI ZA TANZANIA,KENYA,BURUNDI,RWANDA NA UGANDA


Katibu Mkuu wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki DR. Stergomena
Katibu Mkuu wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki DR. Stergomena Taxkizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa rasmi utekelezaji wa soko la pamoja Afrika Mashariki kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Uledi Mussa
Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Uledi Mussa kulia akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari iliyofanyika ofisini kwake leo kulia ni Mhasibu wa Wizara hhiyo Bw. Ahadi Msangi

WAKATI utekelezaji wa Soko la pamoja kwa nchi za Jumuia ya Afrika mashariki unaanza Kesho, WIZARA ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini imewatoa hofu Watanzania kwa kusema kuwa hakutokuwa na uingiaji holela wa wageni kutoka nje kwa kuwa ushirikiano utafuata sheria na taratibu zilizopangwa.

Pamoja na ulegezaji wa mashariti ya uingizaji na utoaji bidhaa nchini, pamoja na kuwepo fursa huru katika utafutaji ajira, Wizara imesema uanzishwaji wa soko la pamoja hauta athiri Sheria na taratibu ambazo zilikuwepo kabla ya uanzishwaji wa ushirikiano.
Fulsa zilizofunguliwa na Tanzania ni pamoja na Walimu wa Vyuo Vikuu elimu ya juu kuanzia mwaka 2010, Sekondari katika masomo ya Hisabati na Sayansi-2011, shule za msingi-2010, walimu wa vyuo vya kilimo-2010, Uhandisi Madini, na Ufundi sanifu-2011, Maofisa Ugani 2015,wauguzi na wakunga- 2010 pamoja na waongoza ndege kuanzia mwaka 2012.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo,Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki Dkt Stergomena Tax alisema, hakuna haja ya Watanzania kuhofia kupoteza chochote kwa kuwa shirikisho halitaendeshwa kwa misingi ya ubaguzi hama wa rangi au utaifa.
Alisema cha msingi ni kwa watanzania wenyewe kutambua na kuchangamkia fursa zitakazojitokeza, ikiwa ni pamoja na kujitahidi kutoa huduma bora zenye ushindani badala ya kutegemea kubebwa na kupendelewa.

"Watanzania tunapaswa kujiamini katika utendaji kazi, wengi tumezoea masuala ya kubebwa na kupendelewa kwa misingi ya kujuana badala ya kutegemea uwezo utendaji kazi, hii ni dhana potofu na tunapaswa kuachana nayo, tusimame wenyewe" alisema Dkt. TAX.

Alisema utekelezaji wa soko la pamoja utakuwa wa Hatua kwa Hatua kulingana na ratiba na taratibu zilizokubaliwa na kuwekwa ndani ya itifaki na nchi wannachama, na kuwa hatua hiyo itatoa nafasi ya kufanyika marekebisho mahala ambapo yatahitajika.
"Utekelezaji wa soko la pamoja utaongozwa na sheria taratibu na kanuni zilizokubaliwa kwa kuondoa vikwanzo ulegezaji wa masharti katika maeneo ya msingi" alisema.
Dkt Tax alisema kuwa upande wa biashara ya bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya jumuiya ya afrika mashariki na kukidhi vigezo vya utambuzi wa asili wa bidhaa zinaweza kusafirishwa kutoka nchi moja hadi nyingine bila kutozwa ushuru wa forodha.
Aidha alisema kuwa kuanzia julai moja Raia wa Afrika mashariki watakuwa huru kuingia na kuishi na kufanya kazi katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya na kupata huduma nyingine kama kutembelea ndugu, matibabu, masomo au utalii, alimradi tu wafuate taratibu zilizowekwa na idara za uhamiaji za nchi husika.
"Ili kunufaika na uhuru huu raia mhusika atawajibika kuwa na hati halali ya kusafiria na kupita katika vituo rasmi mipakani ambako baada ya kukamilisha taratibu za uhamiaji atapewa hati ya kuingia na kukaa nchini kwa kipindi cha miezi sita,"alisema.

Alisema kuwa kwa upande wa ajira raia wa Nchi Wanachama anaruhusiwa kutafuta ajira katika meneo yaliyofunguliwa katika nchi yoyote na kutobaguliwa kwa misingi ya utaifa katika ajira na maslahi na haki nyingine za mfanyakazi.
Alisema kuwa mfanyakazi ataruhusiwa kuambatana na mke wake au mume pamoja na watoto ambapoa nao watanufaika na uhuru wa kuariwa au kujiajiri katika nchi husika.

Alisema katika kuanza kwa biashara ya huduma kwa kunazia nchi wanachama zimekubaliana kuondoa vikwazo hatua kwa hatua na vikwanzo vipya kwa watoa huduma kutoka katika nchi wanachama katika sekta kuu saba za huduma zilizoainishwa

Vilevile alisema kuwa katika soko la mitaji nchi wanachama zimekubali kuondoa vikwanzo kwa raia wa Afrika mashariki kuwekeza kwenye soko la mitaji katika Nchi nyingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hatua kwa hatua kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji.

Alisema kuwa watakuwa na fursa ya kuanzisha na kuendsesha shughuli za biashara na uchumi katika nchi yoyote mwanachama wa jumuiya ya afrika mashariki bila kubaguliwa kwa misingi ya Utaifa wa kampuni au mjasiriamali.
Aidha nchi wanachama imekubali kuandaa orodha ya vikwazo katika sheria zao na kuviwasilisha katika baraza la mawaziri la jumuiya ya Afrika mashariki ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya soko la pamoja kupata nguvu ya kisheria.

Hata hivyo alisema kuwa raia anayetaka kukaanchini anatakiwa kuomba kwa mamlaka husika kibali cha ukazi ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kuingia chini akiambatanisha hati halali ya kusafiria kibali cha kufanya kazi nchini na nyaraka nyingine zitakazo hitajika na ofisi ya uhamiaji.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...