Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, August 4, 2011

TASWA yaandaa Bonanza Maalum la kuwaenzi Wanamichezo waliopata kuiletea sifa nchi kwa kipindi cha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania


Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimeandaa bonanza maalum la kuwapongeza wanamichezo mbalimbali waliopata kuiletea sifa nchi katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Bonanza hilo litafanyika jijini Dar es Salaam Novemba 5, 2011 mahali patakapotangazwa, ikiwa ni kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo kilele chake kitakuwa Desemba 9, 2011.

Kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Juma Pinto kilikubaliana kwa kauli moja kufanya bonanza hilo kwa nia ya kuwatambua wanamichezo hao, kuwapongeza kwa mchango wao, hivyo kuagiza Sekretarieti ya TASWA kushughulikia jambo hilo.

Hivi sasa TASWA inaandaa utaratibu wa kuwaorodhesha wanamichezo hao na kuwatafuta mahali walipo kwa wale ambao bado wapo hai, wakati wale ambao wameshatangulia mbele ya haki baadhi yao familia zao zitahusishwa kwenye shughuli hiyo.

Wanamichezo ambao watapongezwa ni wale walioleta medali mbalimbali kwa michezo tofauti na wale ambao ambao wamepata kuleta sifa kubwa kwa nchi hii katika michuano ya kimataifa.

Pia TASWA ilikubaliana kuwa uangaliwe utaratibu wa sherehe hizo kuwahusisha waandishi wa habari za michezo wa zamani hapa nchini, ili nao kuwapongeza katika sherehe hizo za miaka 50 ya Uhuru, jambo hili bado linafanyiwa kazi ili kuliboresha zaidi.

MAFUNZO YA WAANDISHI CHIPUKIZI


Kamati ya Utendaji ya TASWA inampongeza Mwita Mwaikenda kwa kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) yajulikanayo kama AIPS/FISU Young Reporters' Programme 2011.

Mafunzo hayo, ambayo yatahusisha waandishi wa habari chipukizi yataanza Agosti 12 hadi Agosti 23 mwaka huu huko Shenzhen, China.

Mwita ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la kila wiki la The Express linalotolewa kwa lugha ya Kingereza anatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Jumanne ijayo.

Mwita alipata nafasi hiyo baada ya kutuma maombi kwenye Kamati ya Maandalizi, ya mafunzo hayo kama ambavyo wadau wengine mlijulishwa Mei mwaka huu. Ni matumaini yetu huu ni mwanzo mzuri kwa kijana huyo na TASWA inamtakia kila la kheri na mafanikio mema.

MAFUNZO YA WAANDISHI KWA KANDA


Kamati ya Utendaji ya TASWA imebariki ratiba ya mafunzo ya kitaaluma pamoja na ya michezo kwa wanachama wake kuanzia Septemba mwaka huu.

Semina ya kwanza itafanyika Morogoro Septemba ikihusisha washiriki 50 kutoka Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi, Dodoma na Mtwara. Semina ya pili itakuwa mwishoni mwa Oktoba mkoani Arusha.


Imetolewa na:

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
03/08/2011

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...