Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, February 9, 2012

Asha Baraka aichachafya Mashujaa Band



MKURUGENZI wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka amesema kamwe bendi yake ya Twanga Pepeta International haiwezi kutetereka hata kama wataondoka wanamuziki watano kwa mpigo.
Asha amesema Twanga Pepeta ni chuo cha sanaa na kwamba ataendelea kufanyakazi ya kuwaendeleza wasanii wa Tanzania bila hofu yoyote hadi pale atakapoamua kustaafu kazi hiyo kwa ridhaa yake mwenyewe.
Mkurugenzi huyo wa ASET alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akijibu swali kuhusu sababu za kuishusha jukwaani bendi ya Mashujaa, ilipokuwa ikitumbuiza kwenye viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Asha alisema aliamua kuishusha jukwaani bendi hiyo kwa sababu steji iliyokuwa ikiitumia ni mali yake, hivyo wamiliki wake walipaswa kuomba kuitumia badala ya kutumia ubabe ama kumdharau kwa sababu ya jinsia yake.
"Ile steji ni mali yangu, nimeitengeneza kwa pesa zangu, unapotaka kuitumia ni lazima uombe ili utumie bure ama uikodishe. Isiwe una pesa nyingi ukadhani nitakuogopa, sikuogopi, vinginevyo tengeneza chako,"alisema.
"Unachotakiwa kukifanya ni kuomba, lakini ukichukulia tu kwamba mimi ni mwanamke, atanifanya nini? Au mimi nina pesa nyingi hawezi kunifanya lolote, hapo umechemsha," aliongeza mwanamama huyo, ambaye ni mwanamke wa kwanza nchini kumiliki bendi ya muziki wa dansi.
Asha alisema iwapo kuna mfanyabiashara yoyote anayetaka kununua wanamuziki wote wa Twanga Pepeta, anaweza kufanya hivyo, lakini kamwe hawezi kubadili lolote katika maisha yake.
Mwanamama huyo alisema Twanga Pepeta inaundwa na wanamuziki wengi na kwamba bendi nyingi zilizoundwa miaka ya hivi karibuni kama vile Mapacha Watatu, Mchinga Sound, Extra Bongo na Mashujaa zimetokana na bendi yake.
"ASET inazalisha wanamuziki na tutaendelea kufanya hivyo. Tunao waimbaji 12 na kwa bendi ni wengi sana. Kwa bendi nzima, tunao wanamuziki 34. Hivi karibuni wanamuziki 13 walikwenda Uingereza kwa ajili ya maonyesho ya miaka 50 ya uhuru, lakini hatukusimamisha maonyesho yetu,"alisema.
"Walibaki wanamuziki 20 na waliendelea na maonyesho katika kumbi za Mango Garden, TCC na Leaders. Na wengine walikwenda mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya sherehe kama hizo," aliongeza mwanamama huyo.
"Sisi ni kiwanda cha sanaa, tutaendelea kuwepo na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, waendelee kutuunga mkono na kufurika kwa wingi kwenye maonyesho yetu kama ilivyokuwa wiki iliyopita,"alisema mwanamama huyo.
Akizungumzia tukio hilo, kiongozi wa bendi ya Mashujaa, Yohana Mlawa alisema, hawapendi kuingia kwenye malumbano na bendi ya Twanga Pepeta kwa sababu wanamheshimu mmiliki wake, Asha Baraka kama mdau aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sanaa ya muziki wa dansi nchini.
Hata hivyo, Yohana alisema mwanamuziki kutoka bendi moja hadi nyingine ni si jambo la ajabu na halikuanza kwa mwimbaji Charles Baba, aliyekuwa Twanga Pepeta na kujiunga na Mashujaa na kwamba lengo kubwa huwa ni kutafuta maslahi mazuri zaidi.
"Ukishuka kutoka namba moja hadi mbili, usichukie, jipange upya ili urejee kule ulikotoka,"alisema.
Kiongozi huyo alisema Mashujaa haikumchukua Charles Baba kwa lengo la kuikomoa Twanga Pepeta, bali walifanya hivyo baada ya mwanamuziki huyo kuwaeleza kwamba, hakuwa na mkataba na bendi hiyo.
"Haya yote ni maisha, leo hii yupo Mashujaa, mkataba wake ukimalizika, anaweza kuamua kubaki Mashujaa ama kurudi Twanga Pepeta,"alisema.
Alisema si vizuri kwa wamiliki wa bendi za muziki ama vikundi vya sanaa kuwekeana visasi na kufanyiana vitendo vya kudhalilishana, badala yake wanapaswa kujiuliza chanzo cha tatizo na kulitafutia ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...