KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imetangaza majina ya wasanii watakaowania tuzo za wanamuziki bora nchini za mwaka 2011.
Katika tuzo hizo, vipengele 22 vitashindaniwa na washindi watatangazwa katika sherehe zitakazofanyika Aprili 14 mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Wasanii Isha Ramadhani ’Mashauzi’, Nassib Abdul ’Diamond’, Ally Kiba na Khadija Kopa ndio wanaoongoza kwa kuteuliwa kushiriki kwenye tuzo nyingi zaidi kuliko wengine.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wasanii walioteuliwa kuwania tuzo hizo, wamepitia katika hatua mbalimbali.
Alisema baada ya wasanii kupita katika hatua tofauti, ikiwemo ya mchujo, majaji walikaa chini na kupata wasanii waliopata kura nyingi kabla ya kuhesabiwa na kupata washindi, ambao wameteuliwa kuwania tuzo hizo.
Kavishe alisema jumla ya tuzo 21 zitawaniwa. Alizitaja tuzo hizo kuwa ni mtumbuizaji bora wa kike, mtumbuizaji bora wa kiume, mwimbaji bora wa kiume, mwimbaji bora wa kike, wimbo bora wa taarabu, wimbo bora wa mwaka, wimbo bora wa kiswahili wa bendi, wimbo bora wa R&B, wimbo bora wa hip hop, wimbo bora wa raga na wimbo bora wa dancehall.
Alizitaja tuzo zingine kuwa ni ya rapa bora wa mwaka wa bendi, msanii bora wa hip hop, wimbo bora wa Afrika Mashariki, mtunzi bora wa mwaka, mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka, video bora ya muziki wa mwaka, wimbo bora wa Afro Pop, wimbo bora wa zouk rhumba, wimbo bora wenye vionjo vya kiswahili na msanii bora anayechipukia.
Aliwataja wasanii walioteuliwa kuwania tuzo hizo kuwa ni Khadija Kopa, Isha Mashauzi, Queen Darleen, Dayna na Shaa (mtumbuizaji bora wa kike), Diamond, Ally Kiba, Bob Junior, Dully Sykes na Mzee Yusuf (mtumbuizaji bora wa kiume). Tuzo ya mwimbaji bora wa kiume inawaniwa na Ally Kiba, Diamond, Barnaba, Belle 9 na Mzee Yusuf.
Tuzo ya mwimbaji bora wa kike inawaniawa na Lady Jay Dee, Khadija Kopa, Isha Mashauzi, Dayna na Lina wakati tuzo ya wimbo bora wa taarab inawaniwa na Full Stop (Khadija Kopa), Mamaa Mashauzi (Isha Mashauzi), Hakuna Mkamilifu (Jahazi), Nani kama Mama (Isha Mashauzi) na Nilijua Mtasema (Jahazi).
Tuzo ya wimbo bora wa mwaka inawaniwa na Hakunaga (Suma Lee), Dushelele (Ally Kiba), Moyo Wangu (Diamond), Mathematics (Roma), Nilipe Nisepe (Belle 9) na Riz one (Izzo B). Tuzo ya wimbo bora wa Kiswahili wa bendi ni Dunia Daraja (Africans Stars), Hukumu ya Mnafiki (Mashujaa Band), Falsafa ya Mapenzi (Extra Bongo), Usia wa Babu (Mapacha Watatu) na Mtenda (Extra Bongo).
No comments:
Post a Comment