Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, January 23, 2013

SERIKALI YA ZANZIBAR KUNUSURU KAYA MASIKINI, BALOZI IDD AWAFARIJI WALIOUNGULIWA NYUMBA ZAO


 Jirani wa nyumba no:-497  iliyoungua moto katika mtaa wa Baghani Mjini Zanzibar Bi.Salma Haroub, aliyeshuhudia tukio hilo akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika eneo hilo kuifariji familia ya Bibi Farida Abdulla iliyopatwa na mkasa huo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya sehemu zilizoathiriwa na moto ndani ya nyumba ya Familia ya Bibi Farida Abdulla iliyopo Mtaa wa Baghani Mjini Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua warsha ya siku mbili ya kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati za Uongozi na menejimenti za Tasaf Zanzibar juu ya  mpango wa Taifa wa kunusuru kaya maskini.
  Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki Mh. Waride Bakari Jabu na Mbunge wa Viti Maalum Dr. Maua Abeid Daftari wakiwa miongoni mwa wajumbe wa kamati za uongozi na menejimenti za Tasaf Zanzibar kwenye warsha yao ya siku mbili inayofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Juu wa Tasaf pamoja na Wajumbe wa Kamati za Uongozi na Menejimenti za Tasaf Zanzibar nje ya ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni mara baada ya kuifungua warsha yao ya siku mbili. Hassan Issa – Mpiga picha – OMPR-ZNZ
*********************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imethibitisha azma yake ya kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kunusuru kaya maskini katika Shehia mbali mbali  hapa Zanzibar ili kuondoa umaskini kwa manufaa ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

Mpango huo uliomo ndani ya awamu ya Tatu ya mfuko wa maendeleo ya Jamii Tanzania { Tasaf }  unatarajiwa kuwafikia walengwa wapatao milioni moja na Laki Tano Tanzania Bara na Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kujenga uelewa wa mpango wa Taifa wa kunusuru kaya maskini kwa wajumbe wa Kamati za Uongozi na Menejimenti za Tasaf hapo katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema kwamba ili malengo ya mpango huo yafikiwe na kufanikiwa ipasavyo ushiriki wa wadau mbali mbali unahitajika katika kujizatiti kutekeleza miongozo na taratibu  ndani ya maeneo kwa ufanisi mkubwa.

Alifahamisha kwamba kaya zitakazohusika na mpango huo zitafaidika  kwa kushiriki mpango wa Jamii wa Uhawilishaji Fedha, Miradi ya ujenzi  itayotoa ajira ya muda, miradi ya ujenzi kwa kutoa huduma za Elimu, Afya na Maji pamoja na shughuli za kuweka akiba pamoja na kuwekeza na kujengewa uwezo.

Alielezea matumaini yake kwamba mpango huu wa kunusuru kaya maskini utaimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbali mbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini walengwa ndani ya shehia mbali mbali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza na kuwashukuru washirika wa maendeleo wa Uingereza, Marekani wakiongozwa na Benki ya Dunia { World Bank } kwa kukubali kuchangia mpango huo.  

Akitoa tathmini ya miradi ya Tasaf awamu ya Pili kwa upande wa Zanzibar Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salim Moh’d alisema jumla ya miradi 820 ya maendeleo imetekelezwa ndani ya awamu hiyo ikigharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 12.

Dr. Khalid alizipongeza Kamati  tofauti za Uongozi za Tasaf katika wilaya na shehia mbali mbali za Zanzibar zilizopelekea ufanikishaji mkubwa wa utekelezaji wa awamu ya Pili ya mradi wa Tasaf.

Hata hivyo Dr. Khalid alizitaja baadhi ya  changamoto zilizoleta matatizo ndani ya utekelezaji huo ambazo ni pamoja na soko la bidhaa za wajasiri amali,  Taaluma iliyochangia kutokukamilika baadhi ya miradi pamoja na uwajibikaji mdogo kwa baadhi ya Taasisi ulioshindwa kuratibu vyema awamu ya Pili.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Bwana  Ladislaus Mwamanga alisema dhana ya Mfuko huo katika kupunguza umaskini Nchini ndani ya kipindi cha miaka 12 tokea kuanzishwa kwake haikufikiwa kama ilivyokusudiwa.

Bwana Mwamanga alisema Tasaf awamu ya Tatu inalenga kuwajengea uwezo zaidi watendaji watakaosimamia mpango huo ili kuwafikia walengwa ambao ni Wananchi pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto zote zilizoibuka ndani ya awamu ya Pili ya Tasaf.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika Mtaa wa Baghani Mjini Zanzibar kuifariji Familia ya Bibi Farida Abdulla ambayo ilipata hasara baada ya nyumba wanayoishi kuungua Moto.

Nyumba hiyo iliyo chini ya Kamisheni ya Wakfu na Mali ya amana Zanzibar yenye nambari za usajili 497 iliungua sehemu ya juu ambapo mmoja wa majirani walioshuhudia moto huo Bibi Salma Haroub alimueleza Balozi Seif kwamba chanzo cha moto huo wanafikiria huenda ikawa hitilafu za Umeme.

Bibi Salma alisema kizaa zaa hicho kilisababisha majirani waanze kuchukuwa hatua za kukabiliana na moto huo na baadaye kusaidiwa na Kikosi cha zima moto na uokozi wakifanikiwa kuwaondoa Watoto wawili waliokuwemo ndani ya nyumba hiyo ambapo mzazi wao hakuwepo wakati wa tukio hilo.

Kiongozi Mmoja wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Bwana Abdulla Haji Steni alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wateja wa huduma hiyo kuamuwa kuongeza vifaa tofauti vya umeme bila ya kutoa Taarifa kwenye shirika na wakati mwengine kusababisha hitilafu zinazozaa maafa.

Akitoa nasaha zake mara baada ya baadhi ya wakaazi wa eneo hilo la tukio kutoa shutuma kwa wahandisi wa Shirika la Umeme watati linapotokea tatizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa shirika hilo kuchukuwa hatua za haraka wakati wanaporipotia kutokea kwa hitilafu za umeme.

Balozi Seif alisema zipo kumbu kumbu za matukio kadhaa ya hitilafu za umeme yanayojitokeza na kuripotiwa kwa wahandisi wa shirika hilo lakini utekelezaji wake huchukuwa muda mrefu na kuleta hali ya wasi wasi wa wananachi katika maeneo hayo.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/1/2013.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...