Waamuzi watatu na kamishna mmoja wameondolewa kuchezesha na kusimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na kuonesha upungufu katika uchezeshaji na usimamizi.
Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Februari 11 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za waamuzi na makamishna wa VPL ambayo leo (Februari 12 mwaka huu) inaendelea katika raundi ya 17.
Peter Mujaya wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 101 kati ya JKT Ruvu Stars na Yanga amefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kumudu mchezo huo, hivyo kupata alama za chini.
Naye Isihaka Shirikisho wa Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa VPL msimu huu kwa kushindwa kumudu mchezo namba 105 kati ya Simba na JKT Oljoro. Moja ya udhaifu alioonesha ni kushindwa kumuadhibu mchezaji Patrick Mafisango ambaye alimsukuma baada ya kumuonesha kadi nyekundu Haruna Moshi wa Simba.
Mwamuzi mwingine aliyefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a) ni Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 107 kati ya Villa Squad na Simba. Moja ya udhaifu wa Mapunda ni kushindwa kumpa kadi nyekundu Fred Cosmas wa Villa Squad baada ya kumuonesha kadi ya pili ya njano.
Pia waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa wa Iringa na Kudura Omary wa Tanga waliochezesha mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar wameondolewa katika mechi zilizobaki za VPL kwa kutokuwa makini. Mwamuzi wa mechi hiyo Ibrahim Kidiwa amepewa onyo.
Waamuzi wengine waliopewa onyo na kutakuwa kujirekebisha ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 92 kati ya Moro United na Yanga, na mwamuzi msaidizi wa mechi ya Simba na Coastal Union, Issa Malimali wa Ruvuma.
Kamishna wa mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Mohamed Nyange ameondolewa katika orodha ya makamishna kwa mechi zilizobaki za VPL kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
MAFISANGO AONYWA, SIMBA YAPIGWA FAINI
Kamati ya Ligi imeagiza mchezaji Patrick Mafisango wa Simba aandikiwe barua ya onyo kutokana na kumsukuma mwamuzi Isihaka Shirikisho baada ya kumuonesha kadi nyekundu mchezaji mwenzake Haruna Moshi kwenye mechi kati ya Simba na JKT Oljoro.
Nayo klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kurusha makopo ya soda na chupa za maji wakipinga uamuzi wa mwamuzi Shirikisho kumtoa kwa kadi nyekundu Haruna Moshi.
Wachezaji waliopigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kupiga ambapo pia wanakosa mechi tatu za ligi kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ni nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na Cyprian Lukindo wa Villa Squad.
SIMBA, AZAM ZAINGIZA MIL 67/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Azam lililochezwa Februari 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 67,548,000.
Jumla ya watazamaji 19,257 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 117 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 10,303,932.20 kila timu ilipata sh. 13,182,800.34, uwanja sh. 4,394,266.78.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,757,706.78, TFF sh. 4,394,266.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,197,133.39, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 439,426.78 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 4,394,266.78.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. wamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,350,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,347,990,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 1,555,420.
No comments:
Post a Comment