Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, October 23, 2010

SABODO AENDELEA KUWACHANGIA CHADEMA


MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mustapha Jaffar Sabodo, kwa mara ya pili tena amejitokeza hadharani kukichangia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiasi cha sh mil 100.
Hii ni mara ya pili kwa kada huyo maarufu wa CCM, kutoa kiasi kama hicho, kwani Julai 12, mwaka huu aliichangia Chadema na kuitaka kuendeleza mapambano ya upinzani kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania

Sabodo alikabidhi hundi ya kiasi hicho jana nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam, kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyeambatana na viongozi wa kitaifa akiwemo Mbunge wa viti maalum anayemaliza muda wake Suzan Lyimo na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Antony Komu.

Akikabidhi hundi hiyo, Sabodo alisema licha ya kuwa mwanachama halisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mingi, angependa kuona upinzani na demokrasia ya kweli inaimarika nchini huku akisisitiza kuwa CHADEMA ni chama makini ambacho kitawakomboa watanzania.

Sabodo mmoja wa wazee wanaoheshimika katika jamii kutokana na msimamo wake hata kufikia hatua ya kuikosoa serikali pindi anapoona mambo yanakwenda kinyume hasa kukiuka misingi ya utawala bora, iliyojengwa na mwasisi wa taifa hili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Mimi ni mwanachama wa CCM, lakini napenda kuona demokrasia inakua, huku kambi ya upinzani ikiimarika na kuwa na wabunge wengi bungeni ili kushamirisha maendeleo nchini… leo (jana) nawachangia CHADEMA kwa kwa mara ya pili na ninatambua umakini wenu katika siasa za hapa nchini na hasa bungeni,” alisema Sabodo.

“Nitaendelea kuwa mwanachma halisi wa CCM na nitaendelea kukiunga mkono, lakini bila upinzani kama CHADEMA ilivyo, CCM italala na hakiwezi kuwa makini,” aliongeza mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa kipenzi cha hayati Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.

Katika kuonyesha kuwa CCM kinahitaji kuwa na chama mbadala, mfanyabishara huyo alisisitiza kuwa kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni ni jambo muhimu ili kutoa upinzani kwa CCM na kusukuma maendeleo ya wananchi.

Alisema hali ilivyo sasa nchini ni lazima upinzania uimarike ili kuisukuma serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi waliokataa tamaa na serikali yao huku akisisitiza upinzani sio uadui na kutoa wito kwa wafanyabiashara wengine kulitafari hilo ili kustawisha demokrasia nchini.


HABARI NA PICHA KWA HISANI YA http://bongoweekend.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...