Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, October 20, 2011

MAKAMU WA RAIS DKT BILAL AHUDHURIA SHEREHE ZA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA SAMORA MACHEL-MAPUTO MSUMBIJI:


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,mkewe Mama Zakhia Bilal na Mama Maria Nyerere,wakiwa pamoja na baadhi ya Marais wan chi za Afrika wakati walipohudhulia katika sherehe za maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Mwasisi na Rais wa Mozambiq, Samora Machel, zilizofanyika leo Oktoba 19 mjini Maputo Msumbiji. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.
Askari wakimuongoza Rais wa Mozambiq, Armando Guebuza, kuelekea kuweka Shada la maua katika Kaburi la Mwasisi wan chi hiyo, ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa nchini hiyo, Samora Machel, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Mwasisi na Rais wa Mozambiq, Samora Machel, zilizofanyika leo Oktoba 19 mjini Maputo Msumbiji. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.
Mama Maria Nyerere akiweka Shada la Maua ndani chumba maalum mahala lilipo kaburi la mwasisi wan chi ya Mozambiq, wakati wa maadhimisho ya sherehe za kumbukumbu ya kifo cha mwasisi huyo zilizofanyika mjini Maputo Msumbiji leo Oktoba 19. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA KILELE CHA MAANDHIMISHO YA KUMBUKUMBU YA HAYATI SAMORA MACHEL, NCHINI MSUMBIJI OKTOBA 19, 2011

Ikiwa ni wiki moja tangu Tanzania iadhimishe kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nchini Msumbiji nchi iliyo na mahusiano yasiyo na shaka na Tanzania nayo katika mwaka huu mzima imekuwa katika shamrashamra za kumbukumbu za Baba wa Taifa hilo, Hayati Samora Moises Machel ambazo zimefikia kilele leo, Oktoba 19, 2011 ambapo Tanzania imewakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal.

Katika kumbukumbu hizi, Msumbiji pia imemualika Mjane wa Hayati Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere ambaye yupo pia na mwanaye aliye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere. Wakongwe wengine kutoka Tanzania waliohudhuria siku hii nyeti katika kumbukumbu za harakati za ukombozi wa Afrika ambazo kwa kipindi kirefu ziliasisiwa na Tanzania chini ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni Kingunge Ngombare Mwiru, mwanasiasa mkongwe aliyeweza kutumikia nafasi mbalimbali za kisiasa nchini Tanzania tangu awamu ya kwanza hadi sasa. Pia yupo Brigedia Generali Mstaafu Hashim Mbita ambaye alikuwa Katibu wa kamati ya OAU iliyohusika na harakati za ukombozi wa nchi za Afrika iliyokuwa na makao yake makuu jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Sherehe hizi za kumbukumbu ya Hayati Samora Machel pia zimeangaza katika nchi alizopita na nchi ambazo Msumbiji inaamini zilitoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha ukombozi wake ikiwemo Tanzania. Hayati Samora Machel alifariki kwa ajali ya ndege katika eneo la Mbuzini eneo lililopo katikati ya nchi ya mpaka wa Swaziland, Afrika Kusini na Msumbiji, huku likiwa limezungukwa na milima. Katika milima hiyo ya Mbuzini ambayo kiutawala iko Afrika Kusini, mnamo Oktoba 19, 1986 ndege iliyombeba Rais Samora Machel ilipata ajali na kuangika huku ikisababisha maafa kwa Machel na wenzake 33 na kuacha majeruhi 10 siku ya tarehe 19, Oktoba 1986. Rais Machel alikuwa akitokea Lusaka, Zambia ambako alihudhuria mkutano wa harakati za ukombozi wan chi zilizokuwa Mstari wa mbele na kisha baada ya mkutano huko akaelekea Zaire kukutana na Rais wa nchi hiyo Mobutu Seseko.

Sherehe za jana zilianza kwa Rais wa Msumbiji Armando Guebuza kuelekea katika eneo lilipo kabuli la Hayati Samora Machel maarufu kama Eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa Msumbiji ambapo shughuli hiyo iliambatana na Rais Guebuza kuweka shada la maua katika kabuli la muasisi huyo wa Msumbiji, kisha fursa kama hiyo wakaipata viongozi waalikwa akiwemo Makamu wa Rais Dkt. Bilal. Wageni wengine waliokuwepo ni Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, marais wastaafu wa Zambia Keneth Kaunda, Joachim Chisano wa Msumbiji na Rais wa Brazil Dilma Rousseff ambaye yupo nchini hapa kwa ziara ya kikazi.

Baada ya zoezi hilo umati uliohudhuria ukiongozwa na Rais Guebuza ulihamia katika uwanja wa Uhuru ambapo kazi iliyokuwa ikifanyika hapo ni kuzindua sanamu ya Samora Machel na kisha shughuli ya kitaifa ya kumbukumbu yake kufuata. Waliopata nafasi ya kuzungumza katika shughuli hii ni pamoja na mjane wa Samora Machel, Craca Machel ambaye sasa ni mke wa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Katika hotuba yake ndefu Craca Machel alikumbushia tukio la kufariki kwa mme wake miaka 25 iliyopita huku akitaka serikali ya Msumbiji, Afrika Kusini sambamba na Rais Mugabe kushirikiana katika kusaidia kutoa ripoti yenye kusema ukweli juu ya ajali iliyosababisha kifo cha Machel mwaka 1986.
Ripoti ya awali ya ajali ya ndege hiyo ilieleza kuwa kulikuwepo na matatizo katika ndege huku nyingine ikifafanua kuwepo kwa mawasiliano mchanganyiko kati ya rubani na waongoza ndege. Ripoti zote hizi hazikuwahi kupokelewa na wananchi wa Msumbiji na hisia zimebakia kuwa utawala wa Makaburu wa Afrika Kusini wakati huo ukiongozwa na Pieter Willem Botha ambaye baadaye alijiunga na ANC kuunda serikali ya kwanza ya kidemokrasia nchini Afrika Kusini iliyochaguliwa mwaka 1994 na Rais wake wa kwanza akiwa Nelson Mandela, ulihusika katika kupanga mauaji hayo kufuatia msimamo wa Machel katika kupigania uhuru wa kweli wa wananchi weusi wa Afrika Kusini dhidi ya utawala dhalimu na katili wa Makaburu.
Akihutubia umati wa wananchi wa Maputo na wananchi wa Msumbiji, Rais Guebuza alisema kuwa, Msumbiji kama taifa chini ya uongozi wake itafanya kila iwezalo kuhakikisha ukweli kuhusu mauaji ya Mbuzini unafahamika na kwamba yeye kama kiongozi wa nchi atahakikisha kuwa Msumbiji inabakia moja na kwamba amani iliyopiganiwa na wananchi mbalimbali wa Afrika inadumishwa. Rais huyo pia alifafanua umuhimu wa kuleta mageuzi kiuchumi huku akizungumzia nia njema ya serikali yake katika kukuza demokrasia hasa ikizingatiwa kuwa bunge la nchi yake limeunda Kamati ya kujadili mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo ili iendane na hali ya sasa.
Dkt. Bilal na msafara wake unarejea nyumbani Tanzania kesho baada ya kutembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji sambamba na kukagua kiwanja ambacho kilikabidhiwa kwa Tanzania ili kitumike kujenga ofisi za ubalozi wake hapa Maputo. Kumbukumbu za Rais Samora Machel aliyezaliwa kijiji cha Chilembene Septemba mwaka 29, 1933 zinafanyika sasa wakati Msumbiji na Dunia ikikumbuka miaka 25 ya kifo chake na ni mwaka huu huu ambapo Tanzania inaadhimisha miaka 50 ya uhuru.
Imetolewa na: Boniphace Makene.
Mwandishi wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Oktoba 19, 2011
Mwanasiasa Mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwilu, akijumuika na wananchi wa nchini Mozambiq, kuelekea kuweka mashada ya maua katika kaburi la Mwasisi wa nchini hiyo, wakati wa sherehe za maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa rais wan chi hiyo, Samora Machel, zilizofanyika leo Oktoba 19. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.

Makamu wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Mohammed Gharib Bilal, akiteta jmabo na Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma, wakati walipokutana na katika viwanja vya Mozambiq Heroes Square, kwenye sherehe za maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa nchi hiyo, Samora Machel, zilizofanyika leo Oktoba 19, mjini Maputo. Kulia kwa Makamu ni Mama Zakhia Bilal na (katikati) ni Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma. Picha na Muhidin Sufiani-OMR.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...