Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, October 14, 2011

NCHIMBI AVITAKA VYAMA VYA SIASA KUKUBALI MATOKEO BAADA YA UCHAGUZI


Na Ismail Ngayonga

MAELEZO

Butiama, Mara

VIONGOZI wa vyama vya siasa katika nchi changa duniani hususani za Bara la Afrika wametakiwa kujenga utamaduni wa kukubali matokeo mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kidemokrasia katika nchi zao.

Rai hiyo imetolewa jana kijijini Butiama na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Emmanuel Nchimbi wakati wa mdahalo uliondaliwa kwa ajili ya wakazi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Wizara hiyo.

Dkt. Nchimbi alisema viongozi wa vyama vya siasa katika nchi changa wamekuwa wakitumia muda mwingi kulalamikia matokeo ya uchaguzi mara baada ya washindi kutangazwa badala ya kutumia muda huo kuwaletea maendeleo wananchi.

“Unakuta uchaguzi umekwisha lakini wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanakwenda mahakamani kufungua kesi kupinga matokeo, kitendo hicho kimekuwa kikirudisha nyuma maendeleo, kwa kuwa malalamiko ya uchaguzi huwa hayaishi”, amesisitiza Dkt. Nchimbi.

Kwa mujibu wa Dkt. Nchimbi alisema uchaguzi wa kidemokrasia wa nafasi za uongozi katika nchi inahusisha vyama mbalimbali vya siasa huku kila chama kikiomba ridhaa ya kuongoza wananchi, hivyo vyama vya siasa havina budi kutambua kuwa wenye mamlaka ya mwisho ya kuchagua viongozi ni wananchi.

Aliongeza kuwa kila chama cha kisiasa kina ilani yake ya uchaguzi, ambapo malengo yake ni huwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo yao bila kujali itikadi ya vyama vyao, kwani ilani hiyo huainisha mikakati ya chama mara baada ya kushinda uchaguzi wa kidemokrasia katika nchi.

Aidha alisema iwapo vyama hivyo vya kisiasa havitakubali matokeo ya uchaguzi, ipo hatari kwa taifa hilo kukabiliwa na machafuko ikiwemo vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Katika hatua nyingine Waziri Nchimbi aliwataka wazazi na jamii ya Watanzania kwa ujumla kuwajengea vijana wao utamaduni wa kujitolea kwani hatua hiyo itasaidia kuwajenga kizalendo katika kulipenda, kulilinda na kulitetea taifa lao.

“Kujenga ubinafsi kwa watoto si kitendo kizuri kwani ni hatua ya hupanda mbegu mbaya, taifa letu litaonekana ni taifa la ajabu iwapo vijana wetu watakuwa wabinafsi” alisema Waziri Nchimbi.

Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Butiama, Jackline Seso aliitaka Serikali kuongeza kasi katika vita ya mapambano dhidi ya mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zinazowadhalilisha wanawake na wasichana wadogo katika mikoa mbalimbali nchini.

“Mkoani kwetu Mheshimiwa Waziri kumekuwa na Utamaduni wa ukeketaji wa wanawake na wasichana, kitendo hiki kwa kweli kimekuwa kikitudhalilisha sana sisi akina Mama, tunaiomba Serikali itusadie katika suala hili” alisema Jackline.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...