Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, May 29, 2012

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AKUTANA NA WAZIRI WA MAENDELEO WA FINLAND NA UJUMBE WAKE IKULU DAR ES SALAAM LEO.


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na wa Waziri wa Maendeleo wa nchini Finland, Heidi Hautala (wa pili kushoto kwa Makamu) aliyeongozana na ujumbe wake wakati walipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo asubuhi.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na wajumbe walioongozana na Waziri wa Maendeleo wa Finland, Heidi Hautala (wa pili kutoka kwa Makamu) baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo asubuhi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja kwa kumbukumbu na Waziri wa Maendeleo wa Finland na Ujumbe wake mara baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam, leo asubuhi.
*********************************

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
DKT. BILAL AKUTANA NA WAZIRI WA FINLAND
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na Waziri wa Maendeleo wa Finland Mheshimiwa Deidi Hautala ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano na maendeleo wa nchi hizi mbili.
Katika mazungumzo hayo Dk. Bilal alimweleza Waziri huyo hatua zinazochukuliwa na serikali ya Awamu ya Nne katika kufikia dira ya Taifa ya maendeleo 2025 ikiwa ni pamoja na kutekeleza kauli mbiu ya kilimo kwanza na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Alisema katika kutekeleza kilimo kwanza, serikali inafanya jitihada ya kuhakikisha maafisa ugani wa kutosha wanapatikana ili kusaidia wakulima vijijini kujua mbinu bora za kilimo cha kisasa na namna zitakavyowawezesha kuzalisha kwa tija.
“Hata hivyo, tunajaribu kuongea na taasisi za fedha waweze kuwasaidia wakulima kwa kuwapatia mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao,” alisema na kuongeza
“Tuna tatizo la soko kwani vijiji vingi havijaunganishwa na barabara, bado tunawapa msaada wa kutosha kuhakikisha mazao yao yanafika sokoni. Tunaamini kupitia kilimo kwanza tutawawezesha wakulima wetu kutoka kwenye kilimo cha mashamba madogo na kwenda kwenye mashamba makubwa ya biashara.”
Alipotakiwa kuzungumzia kuhusu mabadiliko ya hivi karibuni ya Baraza la Mawaziri Dk. Bilal alisema hali hiyo inatokana na serikali kutoa madaraka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali na kuruhusu Bunge kuwa huru zaidi.
Makamu wa Rais alimhakikishia Waziri huyo kuwa, wale wote watakaobainika na ubadhirifu wa mali za umma watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kusema kwamba serikali inatambua kuwa Mahakama ni chombo muhimu na kamwe hakuna mwenye mamlaka ya kuingilia katika kutimiza majukumu yake.
Akiwa nchini, Waziri Hautala ambaye anafuatana na ujumbe wa watu 12 anatarajia kuhudhuria mkutano wa Benki ya Maendeleo Afrika utakaofanyika mjini Arusha.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es slaam
Mei 29, 2012

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...