Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, February 27, 2013

ANNA BAYI ATANGAZA KUBWAGA MANYANGA CHANETA



Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Bayi ametangaza rasmi kuwa hatagombea tena ili kutetea nafasi yake wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaofanyika Machi 23 mjini Dodoma.

Bayi amesema kuwa ameamua kung’atuka ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengine wenye sifa kujitokeza na kuongoza chama hicho kwa matarajio ya kuleta mawazo mapya na kuendeleza mchezo huo nchini.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa muda aliotumia kukaa madarakani unatosha kwake na kwamba, anaamini kuwa akishirikiana na wenzake, amesaidia kuipa Chaneta mafanikio makubwa, yakiwamo ya kuipeleka timu ya taifa kushiriki michuano kadhaa ya kimataifa.

"Nimeamua kutogombea tena ili kutoa nafasi kwa wadau wengine kuendeleza gurudumu la netiboli nchini," Bayi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chaneta, Rose Mkisi, aliwasihi watu wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania uongozi katika chama chao.

Mkisi amesema kuwa tangu watangaze tarehe ya kutoa fomu hizo, hakuna mgombea yeyote aliyejitokeza kuchukua fomu hadi sasa, isipokuwa wamepokea taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa baadhi ya wanamichezo kutoka mikoani kuwa wanahitaji fomu za kuwania ujumbe.

"Tunaomba wanamichezo wenye sifa wachangamkie fursa hii ya kuchukua fomu za kuwania uongozi," Mkisi, akiongeza kuwa tarehe ya mwisho ya kurejesha fomu hizo ni Machi 15 na usaili utafanyika Dodoma Machi 21.

Nafasi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo ni pamoja na za mwenyekiti, katibu mkuu, mweka hazina na wajumbe.

Katika hatua nyingine, Chaneta imetaka mikoa kulipa ada ya uanachama kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu kufika

Mkisi amesema mikoa itakayoshindwa kulipia ada ya uanachama haitaruhusiwa kutoa wawakilishi wa kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu.

Awali, uchaguzi wa Chaneta ulikuwa ukipigwa kalenda mara kadhaa kutokana na baadhi ya mikoa kusuasua kuitisha chaguzi zake na pia, baadhi yao kushindwa kulipia ada za uanachama

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...