Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, February 15, 2013

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU DAWA BANDIA



UFAFANUZI KUHUSU TAARIFA ZILIZOTOLEWA KWENYE VYOMBO VYA HABARI NA MITANDAO JUU YA KUINGIZWA NA KUWEPO KWA DAWA BANDIA ZA KUTIBU KIFUA KIKUU

1.  Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini na mitandao ya kimataifa imetoa taarifa juu ya kuingizwa au kuwepo kwa dawa za kutibu ugonjwa wa kifua kikuu (Tuberculosis – TB) zinazohisiwa kuwa ni bandia katika baadhi ya nchi za bara la Afrika ikiwemo Tanzania.

2.   Taarifa zilizotolewa zimeainisha kuwa sampuli zilichukuliwa kutoka kwenye maduka ya dawa binafsi (private pharmacies). Ufafanuzi unatolewa kwamba, dawa za TB huingizwa nchini kwa utaratibu maalum ambapo ni Bohari ya Dawa (MSD) pekee ndiyo hununua na kusambaza dawa hizi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali na baadhi ya vituo binafsi chini ya kibali na usimamizi maalum. Dawa zinazoruhusiwa kuingia nchini ni zile zilizosajiliwa na kuthibitishwa na TFDA. Dawa za kutibu TB haziruhusiwi kuuzwa kwenye maduka ya dawa binafsi.

3.      TFDA inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kuwa taarifa hizo sio za kweli. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mifumo ya ufuatiliaji wa ubora na usalama wa dawa ingeweza kubaini dawa hizo katika soko.  Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, matoleo (batches) 89 ya dawa za TB yaliyochukuliwa kwenye vituo vya forodha (ports of entry) kati ya Januari 2011 na Disemba 2012 na kupimwa kwenye Maabara ya TFDA yameonesha kukidhi vipimo vya Maabara.  Aidha, matoleo 46 ya dawa za TB yaliyochukuliwa kutoka katika vituo vya afya vya Serikali kati ya Juni – Disemba 2012 pia yamekidhi vipimo vya Maabara baada ya kuchunguzwa.

4.      TFDA imeweka mifumo thabiti ya kusajili, kukagua, kuchunguza kwenye Maabara na kufuatilia ubora wa dawa zilizoko kwenye soko. Kupitia mifumo hii, TFDA inaweza kubaini uwepo wa dawa duni na bandia katika soko. Pamoja na mifumo iliyopo, TFDA inawaomba wananchi kutoa taarifa pale wanapokuwa na mashaka kuhusu ubora na usalama wa  dawa za TB  pamoja na dawa nyingine ili hatua stahili zichukuliwe kwa mujibu wa sheria. 

5.      Mamlaka inawashauri wagonjwa wa TB kuendelea kutumia dawa za kutibu ugonjwa huo zinazotolewa bure kwenye vituo vya afya vilivyoruhusiwa na Serikali kwa kuwa ni bora, salama na zenye ufanisi uliothibitishwa na TFDA.

6.      TFDA itaendelea kufuatilia taarifa hizo na kufanya ukaguzi zaidi ili kuhakikisha kwamba dawa za TB zinazotumika nchini ni bora na salama wakati wote.
Kwa maelezo au ufafanuzi zaidi, tafadhali wasiliana na;

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
S.L.P 77150, Dar Es Salaam
Simu: +255 22 2452108/22 2450512
Au:  0658 445222/ 0685 701735/ 0777 700002
Nukushi: +255 22 2450793
Barua pepe: info@tfda.or.tz, Tovuti: www.tfda.or.tz

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...