Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, April 19, 2011

KOCHA WA MCHEZO WA NGUMI SUPER D KUANZA MAFUNZO KWA NJIA YA DVD NCHI NZIMAKOCHA wa ngumi wa Klabu ya Ashanti ya Ilala jijini Dar es Salaam, Rajab Mhamila 'Super D', ameanza kutoa mafunzo ya mchezo wa ngumi kwa wanafunzi wake kwa kutumia DVD.

Akizungumza na Sufianimafoto, Super D alisema kuwa kutokana na maendeleo ya mchezo huo kote duniani ukilinganisha na siku za nyuma, hivi sasa ameamua kufundisha kidijito zadidi.Aidha alisema kuwa baada ya kucheza mchezo huo kwa muda mrefu na kujionea hali halisi ya vijana wanaojihusisha na mchezo huo, kabla ya kuupa kisogo mchezo huo na kuwa kocha wa kuwawezesha vijana, amejiwekea malengo ya kuweza kuwafikisha mbali vijana wenye moyo na mchezo huo..

Akielezea historia yake Super D anasema alianza kujihusisha na huo 1984 baada ya familia yake kupitia baba yake, Mohamed Mhamila 'Checknolis' kuwataka watoto wote kufanya mazoezi kujiepusha na magonjwa kutokana na miili yao kuwa na asili ya unene.

"Baba wakati huo alikuwa ni baunsa akifanya kazi katika kumbi mbalimbali baada ya mazoezi mazito kwa hiyo alipenda na familia yake tuige mfano wake kufanya mazoezi kuweka miili safi tukabukabliana naye.," alisema Super D.

Anasema akiwa Shule ya msingi mwaka 1984 alianza mazoezi katika klabu ya ngumi ya Simba ambako alikutana na watoto wengi wa umri wake na kupata moyo wa kuendelea kuwa hivyo hata mara baada ya kumaliza shule ya msingi na kuwa bondia mkubwa akiwa katika klabu hiyo.

Anasema baba yake huyo ambaye alikuwa ni mpenda mchezo wa mieleka alitoa hamasa kwa watoto wote kufanya mazoezi bila kuchoka na kujikuta wakikubali na kuwa mabondia. wengine ni kaka yake Shaban Mhamila "Star boy, Rashid Mhamila 'Nature Fire' na 'Mohamed Hemed' 'Kadogo Ninja'.

Anasema mjomba wake aliyeitwa Ilak Hudu ambaye alikuwa bondia wa zamani wa mchezo wa ngumi alikuwa akiwavusha barabara ya Msimbazi kwenda katika klabu ya Simba kufanya mazoezi kila siku baada ya muda wa masomo na yeye akiwa miongoni mwao.

Anasema baada ya kupata mafanikio na kucheza akiwa na klabu ya Simba kwa mda mrefu aliamua kujiunga na klabu ya Reli kabla ya kujiunga na Amana lakini kwa wakati huo kipato hakuweza kupata mafanikio makubwa kutokana na msukumo wa mchezo huo kuwa mdogo.

Super D anasema akiwa katika klabu hizo aliweza kucheza na mabondia mbalimbali na kufanikiwa kuwachapa na kuweka rekodi yake vizuri ambao ni Alfred Ngalomba, Husein Pazi, Oscar Manyuka, Safari Benard, Hajibu Salumu, Rajabu Mshindo, Rashid Ally, Mbwana Matumla, na wengine wengi.

"Lakini pia nilichapwa na mabondia bondia Roja Mtagwa kichapo ambacho sitaweza kukisahau na alistahiri kunichapa kwa sababu jamaa anajua na mpambano ulikuwa na upinzani mkari ambapo katika raundi ya kwanza roja nilimdondosha chini na ilipofika raundi ya nne kwenda ya tano nikashindwa kwenda kutokana na kuumia taya hivi sasa anacheza mchezo huu nchini Marekani,." alisema Super D.

Super D aliongeza " Mimi kitaaluma ni mpiga picha nikaamua kujiweka kando kwa muda kufanya mambo mengine kwa sababu mchezo wa ngumi kama ilivyo mingine unahitaji uvumilivu hasa hapa nchini kwetu.," anasema.

Anasema aliacha kucheza mchezo huo mwaka 2002 kutokana na maisha na mchezo wa ngumi kuwa hauna maslahi ya kutosha ukimsababishia kufanya kazi zingine kabla ya kujiunga na kampuni ya Business Times inayochapisha magazeti ya Majira, Spoti Starehe, Maisha, Dar Leo na Business Times akiwa kama mpiga picha akianzia na gazeti la maisha.

Anasema miaka mitatu baadaye alikutana na aliyekuwa kocha wake wa zamani ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kinyogori Foundation, Habibu Kinyogoli ambaye alimshauri aendelee kujihusisha na mchezo huo ndipo alipojiunga kuwa kocha wa klabu ya Ashanti ya Ilala Dar es Salaam baada ya kupata kozi ya awali ya ukocha.

"Nikiwa Ashanti nafundisha watoto wadogo na wakubwa na nashukuru kwa sababu wazazi wa vijana wengi wanauelewa mchezo huu na kuwaleta watoto wao na natumaini watafanya hivyo zaidi.," anasema Super D.

Anasema alijiunga na klabu hiyo miaka miwili iliyopita na mpaka sasa ameweza kufundisha kwa mafanikio ambapo mabondia wake wameweza kushiriki mashindano mbalimbali yakiwemo ya ubingwa wa taifa wa mchezo huo na kufanya vizuri.

Super D anasema kutokana na juhudi zake alizozionyesha Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT) kupitia Kaimu Rais wake Michael Changalawe amemtaka kuhakikisha mabondia anaowafundisha wanafikia viwango kwa sababu klabu yake ni miongoni mwa zinazotegemewa.

"Kutokana na jukumu hilo nililopewa na BFT nimeamua kupanua wigo wa kufanya kazi zangu kuhakikisha nawafikia watanzania wengi na kuelewa mchezo huo wapate kuhamasika ambapo nimeandaa Video CD inayozungumzia maisha yangu nikishiriki mchezo huu zaidi ya mikaka 15 iliyopita na tayari ipo sokoni.," anasema.

Anasema CD hiyo iitwayo Super D Boxing Coach imeanza kuuzwa mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu katika mikoa ya Arusha, Tanga na Dar es Salaam ambapo hadi sasa ameuza nakala 100 katika mikoa hiyo na kwamba anafikiria kusambaza katika mikoa mingine.

Anasema anaamini kuwa kupitia CD hiyo ataweza kufikia lengo la kuwapata mabondia wengi vijana ambao watashiriki mashindano mabalimbali yakiwemo ya Olimpiki ambayo yanatarajiwa kufanyika mwakani London nchini Uingereza.

Anasema video hiyo inaonyesha matukio mbalimbali yanayomhusu tangu alipoanza kucheza mchezo huo mwaka 1984, mapambano aliyocheza na kozi mbalimbali za ukocha wa mchezo huo alizoshiriki wakati akisomea mafunzo ya ukocha miaka michache iliyopita.

Super D amesema pia katika video hiyo amejumuisha matukio mbalimbali ya mabondia maarufu duniani wakiwemo Mike Tyson wa Marekani, Man Pacyao, Mohamed Ali wakiwa ulingoni kutokana na kwamba watakaoshuhudia video hiyo watapata fursa ya kujionea mbinu wanazozitumia mabondia hao wa kimataifa.

Amesema upatikanaji wa Video hiyo ni rahisi ambapo kwa Dar es Salaam inapatikana katika mtaa wa Uhuru na Msimbazi na pia zinauzwa mkononi katika mapambano mbalimbali ya ngumi yanayofanyika Jijini na kuongeza kuwa mabondia wengi maarufu akiwemo Japhet Kaseba, Mada Maugo, Maneno Osward wamenunua na kuiangalia video hiyo.

Super D anasema mbali na filamu hiyo kwa sasa ameanza mpango mwingine ambao kwa kushirikiana na taasisi ya Kinyogori Foundation iliyo chini ya kocha wake Habibu Kinyogoli wameandaa programu maalumu ya kuandaa matamasha kila wiki yanayohusisha mabondia mbalimbali ili kuhamasisha mchezo wa ngumi.

Anasema wanaamini kuwa kupitia programu hiyo vijana wengi wataweza kupata msaukumo kujifunza mchezo huo ambapo kwa sasa programu inaendelea katika Wilaya ya Ilala."Tunazifanya kwa sababu mpira katika soka utakuta watoto wanacheza mpira uwanjani lakini katika ngumi hiki kitu hakipo ndio maana tunaendesha matamasha haya.," anasema Super D.

Bondia huyo alizaliwa mwaka 1977 Ilala Jijini katika hosiptali Ya Ocean Road akiwa ni mtoto wa pili katika familia yao ya watoto wanne na kusoma shule za msingi na Sekondari kabla ya kuendelea na masomo ya juu Jijini Dar es Salaam.


Kocha wa ngumi Rajabu Mhamila 'Super D' akifafanua jambo kuhusu mambo ya msingi yaliyomo katika video yake kwa mabondia Maneno Osward (kushoto na) na Robert Mroso (Wa pili kushoto) pamoja na Chaurembo Palasa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...