Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 26, 2012

KIINGEREZA, UZUNGU WAWAKELA WADAU WA FILAMU ZA BONGO

 Msanii wa filamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Filamu cha Tanzania Film Training Centre (TFTC) Emmanuel Myamba maarufu kama Pastor Myamba akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kushoto kwake ni Katibu wa Shirikisho la Filamu nchini Wilson Makubi
 Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Lebejo akisisitiza jambo wakati akihitimisha programu ya Jukwaa la Sanaa wiki hii.Kulia kwake ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo Agnes Kimwaga
 Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) ambaye pia ni Mratibu wa Kituo cha Mafunzo ya Filamu cha TFTC akielezea kozi mbalimbali zinazotolewa na kituo hicho.
 Mdau wa filamu akihoji uhalali wa matumizi ya lugha ya kiingereza kwenye majina ya filamu za kitanzania.
 Mkongwe wa muziki wa dansi nchini Mzee Kassim Mapili naye alitoa nasaha zake kuhusu tasnia ya filamu.
Sehemu ya wadau wa Jukwaa la Sanaa waliohudhuria wakifuatilia mjadala kwa makini.


Wadau wa Sanaa wamehoji uhalali wa wasanii wa filamu kutumia kiingereza kwenye majina ya filamu zao huku wakishangazwa na kazi hizo kubeba maudhui ya kizungu zaidi.

Wakizungumza wiki hii kwa nyakati tofauti kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa, wadau hao walishangazwa kitendo cha filamu hizo kutumia majina ya kizungu wakati hapa kwetu kuna filamu nyingi kutoka nje zinazotumia lugha za kihindi, kichina, kifaransa  na zinafanya vizuri.

“Hoja kwamba, wanatumia majina ya kiingereza ili kuteka soko la kimataifa ni ya kitoto, mbona hapa kwetu kuna filamu nyingi za kihindi na kichina zinanunuliwa kwa wingi? Hapa kuna udhaifu katika kutengeneza filamu zenye ubora tujikite huko”alisema Mzee Nkwama Bhallanga.

Kwa mujibu wa wadau wengi waliozungumza, filamu ni taaluma inayozungumza kwa kutumia picha na vitendo zaidi hivyo haihitaji mtazamaji kufahamu lugha iliyotumiwa ili afahamu maudhui na ujumbe unaowasilishwa na kazi husika ya filamu.

“Maneno kwenye filamu si muhimu sana, kinachozungumza ni matendo na picha zaidi, ndiyo maana kuna watu wanaangalia picha za Kikorea na wanaburudika na kuelewa kinachoendelea” alisema Godfrey Lebejo ambaye ni Murugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na habari, BASATA.

Aliongeza kuwa, kinachoitesa tasnia ya filamu kwa sasa ni kukosekana kwa weledi na uhalisia wa tamaduni zetu kunakosababishwa na wimbi kubwa la watu kujiingiza kwenye filamu ili kufanikisha mambo yao yaliyo nje ya maadili na utamaduni wetu.

“Inawezekana vipi utengeneze filamu ambayo baba, mama na watoto hawawezi kukaa pamoja kuitazama? Tufike mahali tuseme mambo haya ya kipuuzi basi kwenye filamu zetu” alionya Lebejo.

Awali akiwasilisha mada kuhusu Filamu, wasanii na haja ya kujiendeleza kielimu, Msanii wa filamu Emmanuel Myamba maarufu kam Pastor Myamba alisema kuwa, tasnia ya filamu inakosa weledi hivyo kuhitaji mabadiliko.

“Ni wazi ukiangalia filamu zetu zinakosa weledi katika uandishi wa miswada, uongozaji, uhariri na hata uumbaji wa wahusika. Lazima tukubali udhaifu huu turekebishe” alisema Myamba ambaye kwa sasa amefungua kituo cha mafunzo ya filamu kiitwacho Tanzania Film Training Centre (TFTC) kilichoko Ubungo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...