Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 26, 2012

TGNP wakemea matusi, kejeli na lugha chafu Bungeni

 

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu sana mjadala wa bajeti ya serikali ya mwaka wa Fedha 2012/2013 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumestushwa na kusikitishwa jinsi ambavyo baadhi ya wabunge wanaonesha  tabia ya kutumia nafasi na dhamana waliopewa na wananchi vibaya, kinyume na matarajio.
 
Bajeti ya mwaka 2012/2013 imekuja wakati ambapo wananchi walio wengi wanashuhudia  hali ngumu ya maisha kutokana na mfumko wa bei, ukosefu wa ajira, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, wazee na watoto na kudorora kwa hduma zote muhimu kwa wananchi ikiwemo , maji, afya, nishati, elimu na huduma za kijamii hususani kwa walioko pembezoni. Kwa mantiki hii wananchi wanamategemeo makubwa kwa Bunge na wabunge katika mjadala huo.
 
Kinyume na matarajio hayo, tumesikitishwa na tabia ya baadhi ya wabunge kutumia Bunge kama sehemu ya malumbano ya kisiasa na kutambiana elimu, vyeti na sifa binafsi badala ya kujadili na kufanya maamuzi yenye manufaa kwa nchi yetu.
 
Tumesikia matumizi ya lugha chafu ndani ya Bunge zikitolewa na baadhi ya wabunge, dharau, jeuri, na kejeli badala ya kujadili bajeti kwa misingi ya mahitaji ya  wananchi ambao wanateseka kwa ugumu wa maisha.
 
TGNP tunakemea na kukataa matumizi mabaya ya muda  na nafasi adimu waliopewa wabunge kwa gharama kubwa za wananchi kutumika vibaya, kujadili maisha ya watu binafsi, kushambulia vyama vya siasa, kufanya utani badala ya kujadili jinsi ya kusaidia na kuboresha maisha ya Watanzania waliowengi.
 
Sisi kama wanaharakati na watetezi wa ukombozi wa wanawake, haki za bindamu, demokrasia, na usawa wa kijinsia  tunawataka wabunge na ofisi ya Spika kufanya yafuatayo:
 
  • Kuheshimu kwa dhati muda na gharama za walipa kodi zinazowafanya wawepo Dodoma, mijadala ilenge kuleta tija, mageuzi ya kiuchumi na kubadilisha hali duni  na umasikini wa Mtanzania ambaye amebaki kupata mlo mmoja kwa siku na wengine hawana kabisa.
 
  • Wabunge wajikite kuchambua, kujadili bajeti  na kuishauri serikali namna ya kuboresha na kutekeleza ahadi , mipango yake ya kiuchumi hasa ule wa Miaka mitano (FYDP),MKUKUTA11, Mpango wa Maendeleo(Vision 2025), kwa kurejea Hali halisi ya uchumi wa wananchi kwa sasa iliyosomwa na Waziri wa Nchi (Uhusiano).
 
  • Wabunge kuacha mara moja lugha chafu za matusi, kejeli, dhararu, vurugu na kuchana nyaraka za mijadala Bungeni kwani hiyo ni kuwatusi wananchi walalahoi, ambao ni wapiga kura.
 
  • Spika asiruhusu ushabiki wa  maoni ya mtu binafsi au kikundi bali  hoja za bajeti ya serikali ambayo inawagusa wananchi  wa Tanzania.
 
Kwa kushirikiana  na wananchi  tutaendelea kufuatilia na kudai uwajibikaji  wa wabunge na viongozi  wa serikali katika nagazi zote kwa maendeleo ya Taifa letu. .
 
Imetolewa na:
 
Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...